Makala Maalum: Corona yakosesha akina mama usingizi Makueni

4 min read
Share Button

24 Mei, 2020

Na Mutune Ngumu

Licha ya gharama kubwa ya kuwekeza katika mpango wa upangaji uzazi, taifa la Kenya kama mataifa mengine yanayoendelea kustawi halikusalia nyuma kuanzisha mchakato huu miongo kadhaa iliopita.

Kutoshelezwa kikamilifu kwa mpango huu wa afya bora ya uzazi kwa akina mama kumepigwa kumbo na kuchipuka kwa maradhi hatari ya Covid-19 kutokana na kile wataalamu wa afya wanasema kumechangiwa na serikali na mashirika kuelekeza jududi zake kuangamiza ugongwa huu ulioteka ulimwengu nyara huku sekta zingine muhimu za afya zikitelekezwa kiraslimali na kihuduma.

Mtandao wa www.sharptipnews.com umebaini kuwa imekuwa vigumu wakati huu ambapo serikali imeweka juhudi zake kupigana na Covid-19 kwa wagonjwa wengine haswa wale wanaohitaji kupanga uzazi kupata huduma kutokana na ukosefu wa baadhi ya bidhaa huku wengine wakihofu kufika hospitalini kutokana na ujio wa Corona.

Kwenye mahojiano na Sharptip News, Sarah Mwikali, mkaazi wa mji wa Kibwezi katika kaunti ya Makueni, mzazi
wa watoto wawili anahoji kuwa tangia mwezi wa tatu mwaka huu amekuwa akisaka huduma za upangaji uzazi kwenye kliniki za kibinafsi na zile za umma bila mafanikio kwani sindano ya miezi mitatu anayotumia imekuwa muhali sana na inapopatikana kwenye hospitali za umma huisha kwa haraka kutokana na uhitaji wa wateja huku ile ya hospitali za kibinafsi ikisalia kuwa ghali kutokana na bei yake kupandishwa mara dufu.
“Tangia Machi nimekuwa nikisaka huduma kwenye kliniki na kila mara huwa nafika kuchelewa kutokana na kazi yangu ambayo huwa namaliza kuchelewa…kwa kweli nahofia kuzaa tena licha ya kuwa nina miaka mitano sasa tangia nijifungue mtoto wangu wa
mwisho”, anasema Mwikali.

Kauli sawa na hii ni ile ya Jude Mwende, mkaazi wa mji wa Wote vilevile katika kaunti ya Makueni. Anasema amekuwa mraibu wa kutumia tembe za kupanga uzazi za kila mwezi na kutokana na ujio wa Covid-19 zimekosekana kwenye maduka ya dawa na kila mara zinapokuja huwa chache kumudu mahitaji ya wateja licha ya kuongezwa kwa bei mara dufu.
“Awali ingenigharimu shilingi mia tatu(300) kununua tembe hii ambayo kwa
sasa inapatikana kwa ugumu sana kwa shilingi mia tisa (900). Hata ingawa naweza pata mimba nimeamua kuachana nazo kwa kuwa mume wangu haji kila mara kutokana na janga la Covid-19”, Jude Mwende alitufafanulia.

Takwimu za wizara ya afya kaunti ya Makueni zinaonyesha kupungua kwa idadi ya akina mama wanaozuru hospitali mbalimbali za umma kupata huduma za upangaji uzazi tangia mwezi wa Januari kile kinachoonekana kuchangiwa na hofu ya kuchipuka kwa maradhi hatari ya Covid-19. Mwezi wa Januari uliandikisha idadi ya akina mama wapatao 12,616(61%) waliopata huduma za upangaji uzazi huku Februali ikiandikisha 10,444(54%)
na Machi ikiwa na idadi ya 11,482(55%) katika kaunti hiyo.

Takwimu hizi zinaonyesha kuna asilimia kubwa ya akina mama katika kaunti ya Makueni ambao hawajapata huduma hizi kutokana na sababu moja au nyingine kile ambacho Christine Muindi, msimamizi wa huduma za upangaji uzazi na afya bora kwa akina mama kaunti ya hiyo alidinda kueleza kikamilifu akituelekeza kwenye usimamizi wa wizara.

Bi. Bretta Mutisya(mwenye mkoba), afisa wa kitengo cha kuendeleza afya, Makueni akiwa kwenye mojawapo ya warsha za kuhamasisha jamii mashinani kuhusu afya na upangaji uzazi. PICHA | MUTUNE NGUMU | SHARPTIP NEWS

Kuna uwezekano kuwa huenda akina mama hawa waliokosa kuzuru kliniki za upangaji uzazi wakawa katika hatari ya kupata uja uzito wasioutarajia hivyo kuhatarisha maisha yao, ya wanaowategemea na wanaotarajia kujifungua.

Mwenyikiti wa kamati ya afya kwenye mbunge la kaunti ya Makueni Jaksona Mbalu na ambaye amekuwa kwenye mstari wa mbele kuhamasisha akina mama kujifungulia hospitalini, anahoji kuwa licha ya taifa la Kenya na serikali za kaunti kuangaza macho yake kupigana na Covid-19, pana haja ya washikadau kuratibu mbinu mwafaka kuhakiksha utoaji mwanana wa huduma za upangaji uzazi.

Bi. Ruth Kinya, Msimamizi mkuu wa shirika la kusambaza bidhaa za kupanga uzazi na kuzuia maradhi ya zinaa kaunti ya Makueni la Aids Health Foundation anakiri kuwa kuchipuka kwa maradhi ya Covid-19 kumetatiza pakubwa juhudi za usambazaji bidhaa kutokana na kufungwa kwa vyumba vya burudani, shule, vyuo n.k.

“Corona imetatiza sana juhudi zetu kufikia wateja, ninahisi kwamba huenda idadi kubwa ya akina mama na wasichana waliobalehe ikaadhirika kutokana na wao kuwa kwenye nafasi ya kwanza”, anaongezea Bi. Ruth.

Kwa mujibu wa wizara ya Afya, taifa la Kenya limepiga hatua kubwa katika juhudi za kuboresha afya ya akina mama, watoto wachanga na njia za kupanga uzazi kwa kuwa kuna sehemu zaidi ya akina mama asilimia hamsini na nane(58%) walio kwenye ndoa wanaotumia njia za kisasa za kupanga uzazi haswa wale wanaoishi katika sehemu za mijini ikilinganishwa na wanaoishi mashambani. Hata hivyo huenda juhudi hizi zikalemazwa na kuchipuka kwa maradhi ya Covid-19 kile ambacho serikali inastahiki kuratibu kuhakikisha usawa wa huduma za afya kila wakati kwa kila mmoja.

Kaunti ya Makueni ni baadhi ya kaunti chache ambazo zimepitisha bajeti ya upangaji uzazi huku kila mwaka ikitumia kati ya kitita cha shilingi milioni 20-30 kufanikisha mpango huu ambao sasa umefikia asilimia sitini(60%).

Kama kaunti zingine humu nchini Makueni imepata pigo kutokana na kugeuzwa kwa kituo maalum cha kipekee cha kuhudumia wanarika kuwa kituo cha kupeana matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 kwa muda usiojulikana.

Mwisho.

Facebook Comments
1479
Share Button

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *